Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Kituo cha Uhusiano wa kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim
KONGAMANO LA PILI LA KUMUENZI DKT. SALIM AHMED SAL...

KONGAMANO LA PILI LA KUMUENZI DKT. SALIM AHMED SALIM LIMEFANYIKA JNICC - DAR ES SALAAM

01 Oct, 2026
KONGAMANO LA PILI LA KUMUENZI DKT. SALIM AHMED SALIM LIMEFANYIKA JNICC - DAR ES SALAAM

Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim (CFR) kimeandaa Kongamano la Pili la Kumuenzi Dkt. Salim Ahmed Salim, likilenga kutafakari urithi wake na mchango wake katika diplomasia, ujenzi wa amani na mshikamano wa Afrika.

Kongamano hilo, lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, lilifunguliwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga, kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo.

Akifungua kongamano hilo, Balozi Kasiga amesema Tanzania inatambua mchango mkubwa wa Dkt. Salim katika diplomasia ya Tanzania na kimataifa, hususan katika kuendeleza amani, kusuluhisha migogoro na kuimarisha mshikamano wa Afrika. Aidha, ameeleza kuwa Dkt. Salim amekuwa mstari wa mbele katika kutetea nafasi na maslahi ya nchi zinazoendelea katika mfumo wa kimataifa.

Amesema Dkt. Salim ni miongoni mwa Watanzania walioiwakilisha Tanzania na Afrika kwa umahiri katika majukwaa ya kimataifa, kupitia utumishi wake wa kidiplomasia katika nchi mbalimbali, zikiwemo Misri, India na China, pamoja na Umoja wa Mataifa.

Balozi Kasiga amesisitiza kuwa urithi wa Dkt. Salim unapaswa kutathminiwa kwa kuzingatia pia maadili yake ya utumishi, hekima, busara na mtazamo wake kuhusu nafasi ya Tanzania na Afrika duniani, pamoja na nyadhifa mbalimbali alizowahi kushika.

“Urithi wa Dkt. Salim unatukumbusha nguvu ya maarifa, nidhamu, uadilifu, uvumilivu, kusikiliza na kujenga mahusiano katika diplomasia,” amesema Balozi Kasiga.

Katika ujumbe wake kwa vijana, amewahimiza kuenzi urithi huo kwa kutumia diplomasia kukuza mazungumzo ya amani na kutatua migogoro ndani na nje ya nchi. Amebainisha kuwa njia hiyo inachangia kujenga uaminifu na kuwezesha kupatikana kwa suluhisho endelevu la migogoro.

Vilevile, amewataka vijana kutumia teknolojia mpya, ikiwemo akili unde (AI), kuendeleza maslahi ya Tanzania na Afrika, huku wakizingatia utu, maadili na uwajibikaji.

Kwa kuandaa kongamano hili, CFR imeweka jukwaa la kutafakari mchango wa Dkt. Salim katika historia ya diplomasia ya Afrika na dunia, pamoja na namna mafunzo yanayotokana na utumishi wake yanavyoweza kuongoza kizazi cha sasa katika kuendeleza amani, mazungumzo na ushirikiano wa kimataifa.